JUMA LA MAOMBI TUCASA STUM SOMO LA TATU

ENDELEA KUBALIKIWA
Wednesday, May 24, 2017
SOMO: UTUME NI WETU SOTE.
Mwandaaji: Maregesi January Simula, Mwenyekiti TUCASA SEC 2017/18
Fungu kuu: Mathayo 28:19, 20.  Wimbo namba 107 kitabu kidogo.
SOMO LA JUMA LA MAOMBI: MAY 21-27, 2017  TUCASA STUM


Baada ya kufa kwa Mwokozi wanafunzi walikata tamaa sana na kufa moyo. Jua la 
matumaini katika mioyo yao lilikuwa limekuchwa, na giza ndilo liliwafunika. 
Waliyakumbuka maneno ya Kristo wakiwa katika hali ya ukiwa na upweke kabisa. 
Maneno ya Kristo yalisema hivi; “Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti 
mbichi, itakuwaje katika mkavu?” Luka 23:31
Wanafunzi hali wakijawa na huzuni na majonzi wakiwaza sana kwamba ikiwa Yesu 
waliyemwamini na kumtegemea amefanyiwa hivyo wao je, ni nini kitakachowapata 
wao? Kwa hofu hiyo walikusanyika katika chumba cha juu, wakafunga milango, 
wakiogopa wasipatwe na mambo yaliyompata Yesu. Hapa ndipo Mwokozi alipokutana 
nao baada ya kufufuka kwake na kuwaambia maneno haya “Basi, enendeni, 
mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, 
na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, 
mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Mathayo 28:19, 20
Agizo hilo lilikuwa limetolewa kwa wale wanafunzi kumi na wawili kwanza katika 
chumba cha ghorofa, lakini sasa linatolewa kwa watu wengi zaidi hata kujumuisha na 
kila  Mwana TUCASA  katika jimbo letu kuu la  kusini mwa Tanzania. Wale wanafunzi 
walipokuwa wakitafakari agizo hilo kwa hofu kubwa Yesu aliendelea kusema “Lakini 
mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi 
wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria na hata mwisho wa 
nchi.” Matendo 01:08
Kristo aliwaagiza, wanafunzi wake wafanye kazi aliyowaachia tena kuanzia 
Yerusalemu. Kazi ya wanafunzi ilikuwa lazima ianzie Yerusalemu.  Kumbuka 
Yerusalemu ndipo kilikuwa kitovu cha ibada zote za wayahudi hivyo wale waandishi, 
mafarisayo, walimu wa dini na makuhani akina Kayafa waliokuwa wakimpinga Kristo 
kwa nguvu kubwa walikuwa wenyeji wa Yerusalemu, ukiachilia mbali  askari na  utawala 
wa kirumi kwa ujumla ambao pia ulikuwa kinyume na Kristo. Je,  unaweza kuona kazi 
kubwa  waliyokuwa  nayo wanafunzi wa Kristo kuanzia kazi ya  utume Yerusalemu? 
Wanafunzi wangeweza kuomba mahali pazuri zaidi pa kuanzia kazi, lakini hawakufanya 
ombi kama hilo kwa Yesu.
Siku zote ili kuwa na matokeo makubwa zaidi ya kazi kuna maeneo mawili muhimu ya 
kuanzia kazi hili pia lilifanyika kwa mitume wa Masihi. 
SOMO LA JUMA LA MAOMBI: MAY 21-27, 2017  TUCASA STUM
1.  Eneo la kwanza la kufanyia kazi ni maandalizi ya mtu binafsi kuingia kazini.
Hata wanafunzi wa Yesu walihitaji maandalizi binafsi ya kuingia kazini kwani hata wao 
walikuwa hawajui nini hasa Yesu alikuja kukifanya duniani japokuwa alikaa nao miaka 
mitatu na nusu katika utume, walikuwa bado hawajatambua kusudi la Yesu kwani hata 
maswali yao yalionyesha  hawakujua kusudi la Yesu kuja duniani, “Basi walipokutanika, 
wakamwuliza, wakisema, Je, Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israel ufalme? 
Matendo 1:06 “Yesu akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba 
aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia 
juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na 
katika Uyahudi wote, na Samaria na hata mwisho wa nchi.” Matendo 01:7-8
Maandalizi ya mtu binafsi tunayopaswa kuyafanya ili kuingia  kazini sio jambo lingine 
bali ni yale maandalizi yaliyofanywa na mitume wakati wakingoja ahadi ya kupokea 
nguvu ya Roho Mtakatifu.  Ellen G. White anasema “Katika kutii agizo la Kristo, 
[Wanafunzi] walisubiri katika Yerusalemi kwa ajili ya ahadi ya Baba  ya umwagwaji wa 
Roho. Hawakusubiri wakiwa wamekaa kizembe. Maandiko yanasema kuwa “Walikuwa 
daima ndani ya hekalu wakimsifu Mungu” Luka 24:53. Kwa kadiri wanafunzi 
walivyokuwa wakisubiri utimilisho wa ahadi walinyenyekeza mioyo yao katika toba ya 
kweli, na  kuungama dhambi ya kutokuamini kwao …. Wakiweka kando tofauti zao, 
tamaa yote ya ukuu, walisogeleana karibu sana katika ushirika wa Kikristo” The Acts of 
the Apostles uk. 3537 [1911] anaendelea kusema “Ilikuwa ni baada ya wanafunzi kuwa 
wameingia  katika  umoja halisi, wakati ambapo hapakuwapo tena kushindania 
madaraka ya nafasi ya juu kabisa, Ndipo Roho alipomwagwa.” Testimonies for the 
Church, Vol 8 uk.20 [1904] na anasema tena “Tunapaswa kuomba kwa bidii kwa ajili ya 
kushuka kwa Roho Mtakatifu kama wanafunzi walivyoomba katika  siku ya Pentekoste. 
Kama walimhitaji wakati huo, sisi tunamhitaji  zaidi leo.” Testimonies for the Church, Vol 
5 uk.158 [1882] 
Kwa ufupi  maandalizi hayo na zaidi tunapaswa  sisi pia.  Pale  umoja wa dhati 
utakapoonekana kati yetu  Wana TUCASA  kwa kumthamini kila mmoja wetu bila kujali 
hali za kiuchumi, ngazi gani  ya  kielimu, kozi gani na umoja katika kila jambo 
utakapoonekana, toba na maungamo ya dhambi za wazi na za siri yatakapofanywa, 
tamaa yote ya  mivuto ya kidunia katika  chakula cha kidunia,  mavazi ya kidunia, 
SOMO LA JUMA LA MAOMBI: MAY 21-27, 2017  TUCASA STUM
kutohudhuria  sherehe za kidunia, tamaa za ukuu (uongozi na  madaraka), Usomaji wa 
maandiko  matakatifu utakapohuishwa ndani yetu,  maombi ya dhati yatakapohuishwa 
ndani yetu na mengine yanayofanana na hayo yatakapofanywa kwa dhati, ndipo 
kuburudishwa kwa Roho kutakapoonekana ndani yetu ili tuingie kazini na matokeo ya 
kazi yatakuwa zaidi ya enzi za mitume. 
2.  Anza kazi kwa mtu wa karibu yako kwanza.
Japo kuwa  kuanzia kazi Yerusalemu lilikuwa ni jambo gumu kutokana na changamoto 
tulizoziona hapo awali, Yesu aliagiza sharti kazi ianzie Yerusalemu, Desturi ya Injili 
yenye mafanikio huanzia kwa mtu binafsi na hufuatia kwa mtu/watu wa karibu zaidi 
kuliko wa mbali, tazama jambo hili kwa makini: - “Tena siku ya pili yake Yohana alikuwa 
amesimama pamoja na wawili katika wanafunzi wake. Akamtazama Yesu akitembea, 
akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu! Wale wanafunzi wawili wakamsikia 
akinena, wakamfuata Yesu. Yesu aligeuka, akawaona wakimfuata, akawaambia, 
Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi? 
Akawaambia, Njoni, nanyi mtaona. Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku 
ile. Nayo ilikuwa yapata saa kumi. Andrea, nduguye Simoni Petro, alik uwa mmoja wa 
wale waawili waliomsikia Yohana na kumfuata Yesu. Huyo akamwona kwanza Simoni, 
ndugu yake mwenyewe, akamwambia, Tumemwona Masihi (maana yake, Kristo). 
Akampeleka kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama, akasema, Wewe u Simoni, mwana 
wa Yohana; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro, au Jiwe).” Yohana 01:35 -42.
Tukio la Andrea kuonana na Yesu halikuwa jambo la kawaida, hili lilimfanya amwache 
Yohana na kumfuata Yesu (Hatua ya kwanza imefanyika), wewe umeacha nini na 
kumfuata Yesu? Alipokwisha kumfahamu Yesu mpaka mahali anapoishi alimwona 
kwanza Simoni ndugu yake mwenyewe na kumwambia Tumemwona Masihi (Hatua ya 
pili), Je, umemfahamu na umekutana na huyu Yesu katika maisha yako kiasi cha 
kuanza kuwiwa kutangaza habari zake? Au Je, maisha yako yanadhihirisha   wazi kuwa 
umeonana na Yesu? Ndugu yako wa karibu wa pale chumbani kwako pale ‘Hostel’, 
pale darasani kwako, pale katika kikundi chako cha ‘discussion’ nk Je umempasha 
habari kuwa Umeonana na Yesu? Au mwenendo na matendo yanakusuta  kusema 
habari hizi za Yesu? Kwani hakuna utofauti kati yako na yeye kuwa ni nani aliyeonana 
na Yesu? Zaidi ya kumwambia nduguyo, kifuatacho ni  kumpeleka kwa Yesu kama 
SOMO LA JUMA LA MAOMBI: MAY 21-27, 2017  TUCASA STUM
alivyofanya Andrea (Hatua ya tatu) naye ndugu yako ataitwa jina jipya kwake Yesu 
yaani ataitwa Mwaadventista Msabato kama ilivyotokea kwa Simoni.
Witto:  Wakati wimbo Na. 107 “Sauti ni yake Bwana.” ukiimbwa taratibu kwa sauti ya 
chini kila mmoja ayatafakari maneno ya wimbo huo kwa kina huku mkazo wa kila 
mmoja wetu kuingia shambani mwetu ukiendelea kutolewa.
Mambo ya Kuombea:
1.  Uinjilisti – Kila mwanachama kuleta roho moja kwa Kristo katika mwaka 2017/18.
2.  Roho Mtakatifu na mafanikio ya Global PCM Weekend
3.  Familia zetu, wazazi na walezi.
4.  Viongozi wa kanisa.
5.  Wahitaji na wagonjwa.
6.  Mambo mengine kadri Bwana atakavyowaongoza. 

Comments

Popular posts from this blog

JUMA LA MAOMBI LA VIJANA

MIKUTANO MIKUBWA YA INJILI INAENDELEA KATIKA ENEO LA VITONGA MLALI MOROGORO